Waziri wa Madini Dotto Biteko amebainisha kwamba marekebisho ya sheria ya Madini 2010 yaliyofanyika 2017 yameleta mapinduzi makubwa katika Sekta ya madini nchini kwa kuongeza pato la Taifa na kuvutia wawekezaji.
Waziri Biteko amebainisha haya jijini Dodoma kwenye mdahalo ulioandaliwa na HakiRasilimali kujadili namna gani Serikali inavyoweza kuongeza mapato ya Serikali na kuvutia wawekezaji kwenye Sekta ya uziduaji ikiwa na sehemu ya sherehe za Wiki ya Azaki kwa mwaka huu.
Mdahalo huu ulihudhuriwa na viongozi wengine wa kitaifa wakiwemo Naibu Waziri wa Nishati Stephen Byabato na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Exaud Kigahe ambapo kwa nyakati tofauti walipata fursa kuchangia mada husika kulingana na nafasi zao.
Biteko alieleza zaidi ya kwamba kupitia Sheria hii, wachimbaji wadogo wamepewa nguvu zaidi kushiriki kwenye uchumi wa madini, pamoja na watanzania kunufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi kama vile ajira, ambapo alisema kwa sasa asilimia 96 ya wafanyakazi migodini ni watanzania, na pia asilimia 4 ya watu wanaoshika nyadhifa za juu za uongozi kwenye migodi ni wazawa.
“Baada ya kurekebisha sheria hii Serikali, tumepata manufaa makubwa sana na mapato yameongezeka. Mwaka juzi tulikusanya Sh bilioni 526, na kabla ya mwaka huu wa fedha tumekusanya Sh 586, na Sekta ya madini ikaongoza kwenye Sekta ya uziduaji kwa kukusanya kodi kwa mara ya kwanza,”alisema Biteko.
Aidha kwa upande wa uwekezaji, Biteko alisema ndani ya miaka 15 iliyopita Tanzania haikuwahi kupata mwekezaji wa mgodi mkubwa, lakini baada ya marekebisho ya Sheria ya Madini kufanyika, kwa sasa wawekezaji wamekuja nchini na kufungua migodi mikubwa ukiwamo mgodi wa Nyagaza wa dhahabu ambao utawekeza dola za kimarekani Sh milioni 499 na kuajiri watu 1,200 na utaajiri watu kwenye maeneo yasiyokuwa rasmi watu 300 hadi 500.