Serikali ya Tanzania imesema inategemea mchango mkubwa wa Asasi za Kiraia zinazofanya kazi nchini humo katika utekelezaji na ufuatiliaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo (FYDP III) hususani katika kutoa elimu kuhusu mpango huo kwa wananchi kutokana na kutambua uwezo wao wa kuwafikia wananchi wengi kirahisi.
Haya yameelezwa na mwakilishi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Andrea Aloyce wakati akichangia mdahalo kuhusu FYDP III uliofanyika Jumatatu Oktoba 25, 2021 ikiwa ni sehemu ya sherehe za Wiki ya Azaki kwa mwaka huu zilizofanyika Mkoani Dodoma, Tanzania na kuhudhuriwa na maelfu ya watu wakiwemo wawakili kutoka Azaki, Wabunge, Viongozi wa Serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo.
Aloyce alifafanua zaidi ya kwamba shughuli zinazofanywa na Azaki nchini zimekuwa zinashirikisha jamii hususani wakazi wanaoishi kwenye maeneo ambayo hayafikiki kirahisi kutokana na changamoto kama vile ukosefu wa miundombinu ya barabara, hivyo itakuwa rahisi kwao kuwafikia wananchi wote nchi nzima na kuwapa elimu kuhusu Mpango mpya wa Maendeleo uliozinduliwa mwaka huu.
“Utekelezaji wa FYDP III utagharimu jumla ya fedha kiasi cha Sh114.9 trilioni ambapo Azaki na Sekta Binafsi zinatarajiwa kuchangia Sh40.6 trilioni. Hivyo, ushiriki wenu ni muhimu kuanzia ngazi ya uchangiaji Rasilimali fedha, utekelezaji na ufatiliaji wa mpango huu,” alisema Aloyce.
Lakini hoja hii ya Serikali ilipokelewa kwa mitazamo tofauti miongoni mwa wawakilishi wa Azaki ambao walishiriki mdahalo huo kwani achilia mbali wengi wao kuonyesha kufurashishwa na utayari wa Serikali kushirikiana na nao katika kutekeleza FYDP III, baadhi walitoa mapendekezo kuhusu namna gani ushirikiano wa Azaki na Serikali unapaswa kufanyika ili kufikia lengo lililokusudiwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtandao wa Azaki Mkoani Mbeya, Simon Mwangonda alitoa ushauri kwa Serikali kutoa fedha kwa Azaki nchini ili kuziwezesha kutekeleza shughuli zake ikiwemo kutoa elimu kuhusu mpango huo wa tatu wa maendeleo.
“Hakuna historia ya Serikali ya Tanzania kuzisaidia kifedha Azaki, badala yake imekuwa inazitegemea Azaki ziombe fedha kwa wafadhili halafu ndio zitumie fedha hizo kushirikiana nao katika utekelezaji wa mipango na mikakati ya kitaifa ya maendeleo. Hivyo basi, huu ni wakati sahihi kwa Serikali kuona umuhimu wa kutupatia fedha ili tuweze kushiriki kikamilifu kwenye ujenzi wa Taifa letu,” alisema Mwangonda.