Sekta binafsi nchini Tanzania imesema itatoa takwimu mbalimbali kuainisha maeneo ambayo yanahitaji kuwekewa nguvu zaidi wakati wa utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo (FYDP III) ikiwa ni sehemu ya ushiriki na mchango wake kwenye utekelezaji wa mpango huo mpya.
Haya yameelezwa na Ammi Julian ambaye alikuwa mwakilishi Taasisi ya Sekta Binafsi nchini kwenye mdahalo kuhusu mpango wa maendeleo wa tatu uliofanyika wakati wa sherehe za Wiki ya Azaki jijini Dodoma, Oktoba 25, 2021.
Sura ya tatu ya mpango mpya wa maendeleo umeianisha ushiriki wa Sekta Binafsi na Azaki kwenye utekelezaji wa mpango huo kutokana na kutambua mchango wao katika kujenga Uchumi wa Taifa.
“Achilia mbali ushiriki wetu katika kuchangia fedha za utekelezaji wa FYDP III, pia tuna jukumu la kuandaa takwimu na tafiti mbalimbali kuhusu maeneo ambayo yanapaswa kutolewa macho na mamlaka husika wakati wa utekelezaji wa mpango huu mpya wa maendeleo,” alisema Julian.
Alisema endapo Sekta Binafsi, Azaki na Serikali zitashirikiana kikamilifu, itasaidia utekelezaji mzuri wa mikakati na mipango ya kitaifa ikiwamo mpango wa tatu wa maendeleo ambao umezinduliwa mwaka huu na unatarajia kutekelezwa kwa miaka mitano hadi ifikapo mwaka 2025/26 ukifungamana na Dira ya Maendeleo ya Tanzania – 2025.