Aliyekuwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Profesa Mussa Assad amesema kuna haja ya ofisi ya CAG kuwa na wataalamu wabobezi katika sekta ya madini ili kuimarisha ukaguzi katika eneo hilo.
Katika mdahalo wa kujadili ripoti ya Shirika la Oxfam ambayo inaangazia nafasi ya wakaguzi wakuu wa Serikali katika ukaguzi wa sekta ya madini katika mataifa 10 ya Afrika Profesa Assad amesema kuwa na wataalamu kutaongeza ubora wa ripoti zinazotolewa.
“Wakati mie naondoka ofisini hatukuwa na mjiolojia wala mhandisi wa madini hata mmoja, niliomba mara mbili lakini sikupata,” amesema Profesa Assad.
Ameongeza kuwa “Kutokuwa na wataalamu hao ni tatizo kubwa kwa kawaida ilitakiwa walau wawepo wanajiolojia watano, Wahandisi watano. na wataalamu wa mafuta na gesi watano bila kuwa na wataalamu hao katika ukaguzi ni tatizo kubwa”