Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) Mhe, Japhet Hasunga, amebainisha sababu ya Bunge kushindwa kuchambua ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa wakati, ni kutokana na ratiba ya uwasilishwaji wa ripoti hizo kuingiliana na ratiba za vikao vya Bunge la bajeti vinavyofanyika kila mwezi wa 4.
Hasunga ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Vwawa, amebainisha haya Jumatano Oktoba 27 2021 kwenye mdahalo ulioandaliwa na HakiRasilimali kujadili masuala ya ukaguzi wa mahesabu unaofanywa na taasisi kubwa za ukaguzi wa fedha kwenye Sekta ya uziduaji barani Afrika kiwa ni sehemu ya sherehe za Wiki ya Azaki kwa mwaka huu zilizofanyika jijini Dodoma, Tanzania.
Mjadala uliwahusisha pia CAG wa zamani wa Tanzania Prof Mussa Assad, na Mratibu wa miradi ya Uziduaji kutoka Shrika la Oxfam Adella Msemwa ambaye aliwasilisha matokeo ya utafiti walioufanya kuhusu taasisi za ukaguzi katika nchi 10 barani Afrika, ikiwemo Tanzania, Kenya na Uganda.
“Wabunge huwa tunakosa nafasi ya kuchambua ripoti za CAG mara baada ya kuwasilishwa Bungeni, kutokana na kuwa na majukumu mengine ya kuhudhuria vikao vya bajeti, hivyo hadi tunamaliza Bunge la Bajeti June 30, bado tunakuwa hatujapanga muda kuzichambua ripoti hizo,” amesema Hassunga.
“Mwaka huu tulitaka kuichambua Ripoti ya CAG mapema, lakini tuliwasiliana na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), akatuomba hatuwezi kujadili sababu yeye hajapitia majibu kutoka kwa Maofisa Masuhuli, ili kuthibitisha majibu aliyoyasema kwenye Ripoti yake, na baada ya hapo ndipo tunapata fursa ya kuichambua, mfano Ripoti ya mwaka jana ya CAG ndiyo tumeanza kuichambua Agosti, hivyo tatizo linalocheleshwa kusomwa ni muda tu,”alisema Hasunga.
Akizungumzia kwa upande wa Ripoti za TEITI kutochambuliwa bungeni, alisema taratibu na kanuni za kibunge haziruhusu ripoti hiyo kujadiliwa bungeni. Lakini, Mbunge aliyeisoma hiyo Ripoti anaweza kuitumia kama sehemu ya utafiti wake kutoa mchango bungeni.
Pia alizungumzia mapungufu ya sheria na taratibu ambazo zilikuwa zikimzuia CAG kupata taarifa za kimikataba kwenye Makampuni ya sekta ya uziduaji ambayo serikali ina hisa chini ya asilimia 50. Pamoja na hayo alibainisha kuwa mwaka 2017 Bunge lilifanya Marekebisho ya Sheria ya Madini, yaliyoiruhusu serikali kuwa na umiliki wa hisa usiopungua asilimia 16 hadi 50 kwa kila kampuni kubwa itakayofanya uwekezaji kwenye sekta ya madini.
Katika hatua nyingine, Hasunga amesema kwa sasa Bunge lipokwenye mchakato wa kupitia sheria mbalimbali kurekebisha mapungufu mbalimbali ya kisheria kuhusu Mashirika ambayo Serikali ina Hisa chini ya asilimia 50. Akitolea mfano wa Bomba la Mafuta ghafi kutoka Hoima Uganda mpaka Tanga Tanzania, na kueleza kuwa kwenye mradi huu wanauwezo wa kukaguliwa na Mkaguzi yoyote yule, ambapo kwa sasa wanafikilia kubadilisha utaratibu ili CAG aweze kukagua pia mashirika hayo.
Aidha, akiuliza Swali na kutoa mchango wake juu ya Ripoti za TEITI Mkurugenzi wa Taasisi ya Hakirasilimali, Bi. Racheal Chagonja, alisema mpaka sasa zimezalishwa Ripoti 11, na katika Ripoti za Mlinganisho Tanzania utofauti ni zaidi ya Sh. bilioni 90 fedha ambazo zilipaswa kufanyiwa ukaguzi maalumu wa Mahesabu, na kuishauri Serikali kuwa inapaswa kuweka jitihada za makusudi kuhakikisha kwamba Ripoti hizo (Special Auditing) ziwe zinapelekwa kwenye Kamati, ili kupata ufumbuzi kujua wapi mapato hayo yalipotea.