Ukosefu wa Dira ya Taifa ya Madini nchini Tanzania ni moja ya kikwazo kwa nchi kunufaika na Rasilimali za Madini, Serikali imeelezwa.
Mwanazuoni Japhance Poncian kutoka chuo kikuu cha Dar es Salaam ameyaeleza haya wakati akichangia mdahalo uliofanyika Jumatatu Oktoba 25 jijini Dodoma ikiwa ni sehemu ya sherehe za Wiki ya Azaki kwa mwaka huu zilizokutanisha Asasi za Kiraia mbalimbali nchini.
Poncian aliongeza kwa utafiti ambao ameufanya mwaka huu kwa kupitia Ripoti za Serikali na sheria za Sekta ya Madini zilizopo, amebaini ya kwamba ili kuunganisha mnyororo wa thamani, kuna haja Serikali ya Tanzania kuwa na Dira ya Taifa na siyo kutumia Dira ya Afrika.
“Ushauri kwa Serikali tunapaswa kuwa na Dira ya Taifa ya Madini inayosema wazi wazi juu ya namna wananchi wanapaswa kushiriki kwenye kufanya maamuzi, kutunga Sera, na Sheria kupitia maoni,” alisema Poncian.
Aidha, alisema japokuwa katika bara la Afrika kuna dira ya Madini (AMV), bado kuna haja kwa nchi wanachama kuwa na dira za kitaifa ili kutoa fursa kwa wananchi kushiriki kwenye usimamizi wa mapato yanayotokana na Madini, tofauti na hali ilivyo sasa ambapo wananchi wananufaika kupitia Uwajibikai wa Makampuni kwa Jamii (CSR), ushuru wa huduma (service levy) na ushiriki wao kwenye fursa za kiuchumi kama vile ajira.