UTANGULIZI
Sekta ya uziduaji (madini, mafuta na gesi asilia) ni kichocheo kwa ukuaji wa uchumi wa nchi. Kwa ukubwa wake, sekta hii inakadiriwa kuwa na thamani ya shilingi za Kitanzania milioni 4,975,991. Na huchangia asilimia 4.8 ya Pato la Taifa. Kwa sababu hii, sisi HakiRasilimali-PWYP, jukwaa la Asasi za Kiraia linalochambua sera na kufanya uchechemuzi katika sekta hii nchini Tanzania, tumefuatilia kwa umakini mwelekeo wa kisera na majadiliano na maoni mbalimbali kwa shauku kubwa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Kwa minajili hiyo, tumejadili na kuchambua mwelekeo wa kisera katika sekta hii kwa lengo la kutoa maoni yetu ili kuainisha maeneo yanayohitaji kupewa kipaumbele kwenye Bajeti ya Wizara ya Madini kwa Mwaka 2018/19. Lengo kuu ni kuboresha usimamizi na kuhakikisha kwamba mapato yanayopatika katika sekta hii yanaleta tija itakayochangia kwenye kunufaisha Watanzania kwa ujumla.
MWELEKO WA KISERA
Awali ya yote, tunaipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa uthubutu na msimamo wa kuuhisha mjadala wa kitaifa kuhusu usimamizi wa rasilimali za nchi na manufaa yake kwa umma pamoja na dhamira iliyoonyeshwa ya kuanisha mchakato wa mapitio ya sheria zote zinazosimamia sekta ya madini. Katika jitihada hizi tumeona mabadiliko yafuatayo:
- Muundo wa Wizara: Katika kuongeza ufanisi katika sekta ya uziduaji, Wizara ya nishati na madini mwaka wa fedha 2017/18 iligawanywa na kuwa wizara mbili; wizara ya Nishati na Wizara ya Madini, ambapo Wizara ya Madini ina idara tatu (3) (sera , mipango na idara ya madini) kwa ujumla wake wizara ina vitengo sita (6) na taasisi sita (6); Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji-TEITI, Chuo cha Madini, Kituo cha Jemolojia Tanzania, Shirika la Madini la Taifa-STAMICO na Tume ya Madini. Mgawanyo huu utasaidia kuongeza ufanisi katika ukusanyaji mapato kutoka vyanzo mbalimbali kupitia taasisi za Wizara na vilevile kuboresha matumizi hasa katika kuboresha uwezo wa usimamizi wa sekta hii muhimu.
- Utekelezwaji wa sheria nchini: Miongoni mwa majukumu yake, Wizara ya Madini inapaswa kubuni, kuandaa na kusimamia sera, sheria, mikakati na mipango katika sekta ya madini. Lakini pia kusimamia na kuhamasisha shughuli za uchimbaji na utafutaji wa madini. Marekebisho ya sheria: Kwa mwaka wa fedha 2017/18, tumeona kufanyika kwa marekebisho ya sheria ya madini ya mwaka 2010 kupitia Sheria ya Marekebisho Anuai ya Sheria Na. 7 ya Mwaka 2017 ambayo imepelekea ongezeko la mirabaha kutoka asilimia nne (4) hadi sita (6); kutungwa kwa kanuni za kukuza ushiriki wa wazawa (2018), lakini pia kuundwa kwa tume ya Madini.
- Ulizi wa rasilimali madini: Mwaka wa fedha 2017/18, tumeshuhudia ujenzi wa ukuta wa kilomita za mraba 15 kuzunguka eneo la Mererani na kulinda madini ya adimu duniani ya Tanzanite ili kuwezesha upatikanaji wa kodi itokanayo na mauzo ya madini hayo kwa urahisi.
- Mpango wa uhamasishaji uwazi na uwajibikaji Tanzania: Mpango wa uwazi na uwajibikaji Tanzania katika sekta ya mafuta, gesi na madini uko chini ya sheria ya Uwazi na Uwajibikaji ya mwaka 2015 unaongozwa na mwenyekiti huru na wanachama kutoka mashirika ya kiraia, makampuni na Serikali. Kikundi hiki kinahakikisha kuchapishwa kwa ripoti ambazo zinazopatanisha malipo ya kampuni na mapato ya serikali kutoka sekta ya ziada. Kwa kipindi cha miaka mitatu (3) ya utekelezaji wa sheria ya Uwazi na Uwajibikaji, Sheria hii, imeweza kuongeza uaminifu wa data kwenye sekta, hasa katika machapisho ya ripoti za uwazi na uwajibikaji kuhusu malipo, mapato, uzalishaji, utawala wa kisheria na fedha, makampuni ya mafuta na gesi, upatikanaji na uaminifu wa data kwa kutoa ripoti kila mwaka ambayo inapatikana kwa umma kupitia tovuti ya taasisi ya uwazi na uwajibikaji (ripoti ya nane hadi sasa inayoonesha makadirio ya mwaka wa makusanyo 2015/16). Mbali na hilo, tunapongeza jitihada za serikali katika kutatua changamoto zilizojitokeza kwa mfano uwakilishi wa asasi za kiraia (PWYP) katika mpango wa Uwazi na Uwajibikaji (TEITI-MSG)
Hata hivyo TEITI imekua ikitengewa pesa kidogo sana kutoka serikali na kutegemea ufadhili mkubwa kutoka kwa wa hisani kutoka nje ya nchi kitu ambacho kinafanya kazi za tasisi hii kususua na kukosa uhakika haswa wakati hu ambao mchango ya wafadhili kutoka nje yote imekwisha.
CHANGAMOTO KATIKA UTEKELEZAJI WA SHERIA
Licha ya jitihada zilizofanywa na zinazoendelea kufayika katika kuboresha sekta hii, mfumo wa kisheria, licha ya kuwa na idadi ya sheria zinazohusu masuala yanayohusiana na umiliki wa manufaa, haitoshi katika ufanisi wa masuala ya kukabiliana na matatizo na changamoto zinazosababishwa na ukosefu wa kutoa taarifa ya kuridhisha kwa sababu zifuatazo:
- Usimamizi: Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji kwa muundo mpya, itasimamiwa na Wizara ya Madini. Ndani yake ikiongelea uwazi na uwajibikaji pia katika maswala ya nishati nchini. Kwa mantiki hiyo, muundo huu mpya haujatoa vielelezo vya kutosha namna gani sheria hii imegawanya majukumuu kati ya wizara mbili yaani Wizara ya Madini na Wizara ya Nishati.
- Kanuni: Sheria hii inalenga kuongeza uwazi na uwajibikaji katika sekta ya madini, mafuta na gesi nchini. Chakushangaza, hadi sasa sheria hii imekua ikifanya kazi bila kuwepo kwa Kanuni na Taratibu jinsi gani sheria inaweza kutekelezwa.
- Uwazi wa mikataba na umiliki wa makampuni: Kusudi kuu la Sheria ya uwazi na uwajibikaji ni kutoa ufafanuzi kamili wa uwazi wa mikataba na mmiliki katika makampuni ya sekta ya uziduaji Tanzania. Sheria inataka kuwepo utaratibu wa kufungua/ kuweka wazi mikataba (MDAs na PSA) na kuainisha wamiliki halali wa makampuni wanaonufaika kutoka kwa serikali na makampuni husika. Kwa kujua wamiliki wa mwisho wa kampuni, shughuli za sekta ya madini na uziduaji kwa ujumla zitaweza kuwa wazi zaidi. Hata hivyo sheria inatoa mwanya mbaya kwa kumpa mamlaka Waziri kuweka wazi majina ya wamiliki wa makampuni badala ya makampuni yenyewe hivyo kuruhusu jambo liwe la MAAMUZI ya MTU BINAFSI badala ya takwa la kisheria. Lakini pia mfumo huu wa kisheria hauna uwezo wa kutosha katika kukabiliana na masuala na changamoto kwa ufanisi kutokana na kukosa taarifa ya kutosha katika sekta ya madini, mafuta na gesi nchini. Mbali na hivyo hakuna kanuni zinazoelezea uwazi na umiliki katika sekta ya madini
MAKADIRIO YA MAKUSANYO KWA MWAKA 2018/2019
Uchumi wa nchi unaonekana kukuwa kwa wastani wa 6.8% Katika kipindi cha robo tatu za mwanzo za mwaka wa fedha 2017/2018, na shughuli za madini zikionekana kukuwa kwa kasi zaidi kwa 24.3% ukiliganisha na sekta nyingine. Kutokana na ukuwaji huo wa kasi na mwenendo wa kibajeti hususani kwa makusanyo yanayofanywa na wizara husika kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita, inatoa muelekeo wa ongezeko la ukusanywaji wa mapato katika sekta na wizara husika kwa mwaka 2017/2018. Kati ya mwaka wa fedha 2015/2016 iliyokuwa Wizara ya Nishati na Madini ilikusanya asilimia 75 ya makadirio yake na kwa mwaka 2016/2017 makusanyo yalikuwa asilimia 72 ya makadirio yake. Lakini pia, tumeona punguzo la asilimia katika changio kutoka kwenye sekta ya uziduaji kwenda kwenye bajeti ya taifa mwaka wa fedha 2017/18.
Waziri Mkuu wakati akiwasilisha bungeni hotuba kuhusu mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali kwa Mwaka 2017/2018 alisisitiza kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2017/2018 maduhuli ya Serikali yaliyokusanywa kutoka katika sekta ya madini yalifikia shilingi bilioni 180.4. Pia Serikali iliendesha zoezi la ukaguzi na kuwezesha kukamatwa kwa madini yaliyokuwa yakitoroshwa yenye jumla ya thamani ya Dola za Marekani takriban 898,523 na shilingi milioni 557 ambayo yalifanyiwa mnada hapahapa nchini.
Lakini pia, mwaka huo huo, Serikali kupitia wizara ya Nishati na Madini, ilikuwa na vipaumbele mbalimbali vilivyolenga kuhakikisha nchi inapata mapato sahihi yatokanayo na madini. Katika kuhakikisha hilo, Aprili 2018, Serikali ilizindua ukuta uliozunguka machimbo ya Tanzanite kwa lengo la kuimarisha udhibiti wa utoroshwaji wa madini na kuhakikisha Serikali haipotezi mapato kutokana na utoroshwaji wa madini aina ya Tanzanite kwa njia zisizo halali. Mbali na hilo pia kulifanyika mnada mkubwa wa Tanzanite yenye uzito wa gramu 47,201 iliouza kwa shilingi 1,839,476,075 (ilioipatia serikali mrabaha wa shilingi millioni 110.3 kama ada ya ukaguzi). Makusanyo mengine mbali na bajeti iliyopangwa na Serikali kwa mwaka wa fedha 2017/18 yalitokana na mazungumzo yaliyofanywa kwa niamba ya umma kati ya serikali na kampuni ya Acacia, iliyotoa kiasi cha dola za Kimarekani milioni 330 kwa lengo la kukomesha mgogoro ambao ungepinga shughuli zake nchini.
Aidha, Mwenyekiti Mtendaji wa Barrick Gold John Thornton, alisema kampuni hiyo ya madini itatoa kwa Tanzania hisa za asilimia 16 katika migodi yake mitatu (3) na asilimia 50 katika makusanyo ya mapato katika migodi hiyo.
Tegemeo letu ni kuona ongezeko la bajeti kwa mwaka wa fedha 2018/19. Lakini pia kupata ufafanuzi kwa namna gani makusanyo yaliofanyika nje ya bajeti iliopitishwa mwaka 2017/18 yametumika katika miradi ya maendeleo nchini
TEITI ni taasisi muhimu katika usimamizi wa madini na tunaamini haijatengewa rasilimali fedha za kutosha tangia kuundwa kwake ili kufanya shughuli zake kwa ufanisi. Ukiachia shughuli muhimu inayofanywa kila mwaka kutoa ripoti ya malipo kutoka kampuni za madini, mafuta na gesi asilia, bado kazi kubwa ya kuhamasisha na kujenga uwezo wa wananchi kufuatilia mapato yatokanayo na rasilimali hizi ihitajika. Halikadhalika kwa mwaka wa fedha 2018/19, wadau wa sekta nzima ya uziduaji wanatarajia Rejista ya wamiliki wa kampuni za madini, mafuta na gesi asilia ambayo imekuwa ikisubiriwa kwa shauku kubwa itaanzishwa na kuwekwa wazi kwenye tovuti ya wizara ili kusaidia mapambano dhidi ya ukwepaji kodi na rushwa.
Licha ya kwamba Sera ya Madini ya 2009 inagusia umuhimu wa ushirikishwaji wa wanawake kwenye shughuli za uziduaji na kujengewa uwezo, bajeti za miaka iliyopita za Wizara hazijawahi kuainisha fedha zinazotengwa kwa ajili ya utekelezaji huu. Inakadiriwa kuwa watanzania milioni moja wamejiajiri au kuajiriwa kwenye sekta ndogo ya wachimbaji wadogo na takribani asilimia 25 ni wanawake. Wanawake wapo katika machimbo ya chumvi (38%), uziduaji wa madini ya ujenzi (32%) pamoja na dhahabu na almasi (37%) ila asilimia 10 ya wanawake wana leseni za uchimbaji madini. Sekta hii ndogo pia inakadiriwa kuleta ajira kwa watanzania milioni 7 ambayo ina idadi kubwa ya wanawake.
CHANGAMOTO:
- Udangayifu kupitia gharama za vifaa / huduma –Mispricing: Njia nyingine kubwa inayotumiwa na makampuni ya uziduaji hapa nchini kukwepa kodi ni kupitia mbinu ya udanganyaji wa gharama za vifaa au huduma (mispricing) makampuni ya uziduaji hutumia mbinu hii kwa kuonesha gharama isiyohalali ya vifaa vinavyoagizwa kutoka nje hasa kutoka kwenye makampuni tanzu na hivyo kukwepa kodi na Serikali hukosa kupata mapato stahiki.
- Bado kunachangamoto kwa serikali kuudhibitishia umma endapo viwango vya Mapato yanayotolewa na makampuni ya uchimbaji nchini Tanzania ni sahihi na yanausawa/haki. Ugumu huu wa usahihi wa malipo unatokana na usiri wa ajabu na usio walazima katika uingiaji wa mikataba baina ya makampuni na wakala za serikali. Pamoja na uwepo wa sheria zinazotoa miongozo ya kodi zinazotakiwa kulipwa na makampuni bado kunahaja ya kuweka wazi mwenendo mzima wa uingiwaji wa mikataba hii na nini hasa kipo kwenye mkataba kuweza kufanya ufuatiliaji wa karibu na kupata mapato yaliyosahii na sawa kwa taifa.
- Kutokuwepo kwa ufafanuzi rasmi wa maana ya maslahi ya nchi kumesababisha kukosekana kwa uwiano kati ya haki za jamii zinazozunguka maeneo migodi kukosa nguvu dhidi ya kinachoitwa National interest.
MAPENDEKEZO YA VIPAUMBELE MWAKA 2018/19
- Kutengwe rasilimali fedha za kutosha kuhakikisha Tanzania inaelekea kwenye uwepo wa mpango thabiti na huru wa Uwazi na Uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali za nchi (TEITA), ambao unashirikisha wadau mbalimbali, pia kutambuliwa vizuri ndani ya serikali kuwa Asasi za Kiraia zina mchango mkubwa katika kukuza uelewa wa umma kuhusu mapato ya serikali yatokanayo na sekta ya madini pamoja na uhalisia wa kufikiwa kwa matarajio.
- Utekelezaji wa masuala mtambuka kama ya jinsia. Wizara ya Madini kupitia STAMICO itenge fedha za kujua idadi ya wanawake wanaojihusisha moja kwa moja na shughuli za madini nchini ili kuwa na taarifa sahihi zitakazosaidia kupambana na masuala ya unyanyasaji wa kijinsia kutoka kwa wafanyabiashara, wamiliki wa migodi na wafanyakazi wengi.
- Serikali itoe ufafanuzi kwa namna gani makusanyo yaliofanyika nje ya bajeti iliopitishwa mwaka 2017/18 yametumika katika miradi ya maendeleo nchini.
- Serikali itafute mbinu za mbadala ya kuvutia makampuni ya uchimbaji Madini nchini badala ya kutoa motisha za kodi na misamaha ya kodi. Serikali ipitie sheria na kupunguza motisha na misamaha ya kodi kwa makampuni yanayojishughulisha na uchimbaji wa madini. Serikali inaweze kutumia mikakati mingine kuvutia wawekezaji katika sekta ya madini kama vile usalama, utulivu wa kisiasa, kuimarisha miundo mbinu, kuondoa urasimu katika ngazi zote za utekelezaji.
- Uwazi na uwajibikaji wa Serikali katika sekta ya uziduaji utawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kufanya maamuzi kikamilifu juu ya mapato yanayotokana na sekta hii. Hii inaweza kufanikiwa tu pale ambapo mipango ya uwekezaji na biashara ya Serikali itafanyika kwa uwazi ili wadau waweze kuichambua sekta ipasavyo. Kwa hiyo Serikali kupitia Bunge iweke mikakati ya kuweka michakato ya mikataba wazi
- Ili Serikali iweza kufikisha malengo inayojipangia katika ukusanyaji wa mapato katika sekta ya madini nchini inatakiwa kuimarisha misingi yakukusanya mapato.
-
- Kuwepo na mpango wa udhibiti wenye tija katika utoaji wa lesini za utafutaji na uchimbaji wa madini kwa divisheni zote.
- Kuwepo mfumo utakaowezesha upatikanaji wa taarifa sahihi za bei elekezi za madini nchini, Ilikupunguza wimbi la soko haramu
- Kutengenezwe kanuni mahususi kwa ajili ya kusimamia minada ya madini nchini
- Kutenga bajeti kwa ajili ya kuimarisha kazi ya Mpango wa Taifa takita kutekeleza Uwazi na Uwajibikaji (TEITI)
- Serikali ifuatilie na kutoa ufafanuzi wa uhakika kuhusu kiasi cha 33bln kati ya pesa iliyolipwa na makampuni na kiasi kilichopokewa na serikali kama inavyonyesha kwenye ripoti ya TEITI
- Kuhimarisha mfumo wa uhakiki wa kiasi cha madini yaliyovunwa, kusafirishwa na kuuzwa nje ili kubaini uhakika wa tarifa za mapato na kodi iliyolipwa na makampuni
- Kuimarisha ufuatiliaji na usimazi wa ufungaji wa migodi na kurejesha maeneo ya migodi iliyofungwa kwenye hali ya mazingira masafi
- Serikali isimamie na kuhakikisha manufa ya wananchi kwenye maeneo yanayozunguka kwenye migodi.
- Serikali iainishe baadhi ya huduma muhimu za kijamii ambazo zitapewa kipaumbele kwenye mpango wa CSR wa kila kampuni kama vile barabara, maji, umeme, huduma ya afya na elimu badala ya kuziachia kampuni kufanya yale wanayotaka kwa wakati wanaoutaka na kwenda tofauti na malengo ya Serikali.
- Serikali ifanye uhakiki wa madeni ya mikopo yanayotangazwa na wawekezaji kisha kuingizwa kwenye gharama za mtaji, bila kudhibiti jambo hili hakuna siku Tanzania itapata gawiwo la faida katika miradi inayostahili gawiwo.
Tamko hili limeandaliwa na HakiRasilimali-PWYP. Kwa habari zaidi tafadhali wasiliana nasi: info@hakirasilimali.or.tz /+255 745 655 655