Taarifa mbalimbali zimekuwa zikieleza kuwa sekta ya madini hapa nchini inakua kila mwaka lakini pengine ukuaji huo umekuwa hauonekani kwa wananchi jambo ambalo linaibua swali juu ya uhusiano uliopo kati ya ukuaji wa sekta hiyo na maisha ya watu.
Lakini swali hilo huenda likapata majibu kesho Oktoba 25, 2021 wakati wa warsha kuhusu Usimamizi bora na endelevu kwa ajili ya ukuaji jumuishi. Tukio hilo lililoandaliwa na asasi ya HakiRasilimali litafanyika jijini Dodoma ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya Azaki 2021.
Meneja uchechemuzi na ushirikishaji wa taasisi ya Policy Forum, Elinami John anasema licha ya maendeleo na ukuaji unaotajwa yeye bado hajaona umegusa vipi maendeleo ya mwananchi mmoja mmoja hususani wa maeneo ya karibu na shughuli za uchimbaji. “Matarajio yangu katika warsha hiyo changamoto zitajadiliwa zinazowafanya wananchi wasiwe sambamba na ukuaji huo pamoja na nini kifanyike ili kama kuna mabadiliko ya sheria au ya sera yafanyike ili wananchi wanufaikae,” amesema.
Ameongeza kuwa kuna haja ya kuwa na dira ya madini ya taifa na kutathimini nini kifanyike kuongeza uwazi zaidi kwa kuweka wazi taarifa za mapato na mikataba inayoingiwa ili kuongeza uadilifu.
Katika warsha hiyo kuhusu Usimamizi bora na endelevu kwa ajili ya ukuaji jumuishi wazungumzaji wanatarajiwa kuwa Terrece Ngole kutoka Wizara ya Madini, Erick Luwongo wa HakiMadini, Mbunge Jesca Kishoa na Japhace Poncian wa Chuo Kikuu cha Mkwawa.