Mbunge wa jimbo la Busanda mkoani Geita, Mhe. Tumaini Magessa amesema kuna haja ya kuwa na kampeni ya nchi nzima kuhamasisha ufungamanishaji wa sekta ya madini na sekta nyingine hususani kilimo ili kuwa na uchumi endelevu.
Magesa amesema hayo Oktoba 24, 2021 wakati alipotembelea banda la asasi ya HakiRasilimali wakati wa maonyesho ya Wiki ya Azaki 2021 ambayo yanaendelea jijini Dodoma.
“Katika maeneo ninayotoka shughuli za uchimbaji wa dhahabu zimekuza miji na kuimarisha biashara. Pesa inayopatikana kwenye uchimbaji imeimarisha na kuibua biashara nyingine zikiwemo za maduka”, amesema Mhe. Magessa.
Ameongeza kuwa, “Licha ya biashara hizo zilizoibuka lakini eneo la kilimo bado haliridhishi, bado pesa zinazotoka kwenye madini hatujaweza kuzipeleka kwenye kuinua kilimo ambacho ndicho nguzo kuu ya uchumi. Hili ni jambo ambalo linapaswa kuwa kampeni ya nchi nzima katika maeneo yenye shughuli za uchimbaji”.