Asasi za Kiraia zinazofanya shughuli za kimkakati kwenye Sekta mbalimbali nchini Tanzania zimeeleza kuridhishwa na namna ambavyo imeshirikishwa na Serikali wakati wa zoezi la uandaaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo (FYDP III 2020/21 – 2025/26.
Reynald Maeda kutoka Asasi ya Umoja wa Mataifa Tanzania (UNA) alithibitisha hili wakati akichangia mdahalo kuhusu FYDP III uliofanyika Jumatatu Oktoba 25, 2021 katika Ukumbi wa Royal Village jijini Dodoma, Tanzania.
Alisema hii ni mara ya kwanza kwa Serikali kuzishirikisha Sekta Binafsi na Azaki wakati wa uaandaaji wa mpango huu muhimu wa kitaifa wa maendeleo, na kuongeza kwamba hatua hiyo itasaidia kuongeza ushiriki wao kwenye hatua ya utekelezaji wa mpango huo ambao ulizinduliwa nchini mwaka huu.
Maeda ambaye alikuwa ni miongoni wa wazungumzaji wakuu wakati wa mdahalo akiwa kama mwakilishi wa Asasi za Kiraia nchini ambapo aliwataka Azaki nchini kutokuwa na hofu yoyote juu ya ushiriki wao kwenye uaandaji na utekelezaji wa FYDP III.
“Moja ya maeneo ambayo tumeshiriki wakati wa uaandaaji wa mpango huu ni pamoja na kuingiza Takwimu zilizozalishwa na Asasi za kiraia kwenye Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kuhusu utekelezaji na ufuatiliaji wa mpango,” alisema Maeda.